Wednesday, July 6, 2016

Rais Magufuli Amwaga Burungutu la Fedha Kusaidia Safari Ya Hija.........Pia Kaahidi Kurejesha Mali za Waislamu Zilizodhulumiw


Rais John Magufuli amemwaga burungutu la fedha kusaidia Waislamu ambao watakwenda kuhiji Agosti mwaka huu. 
“Najua kuna Waislamu watakwenda kuhiji nadhani Agosti, naomba kama inaruhusiwa na mimi nichangie kitu kidogo kadri ya uwezo wangu, nimejipigapiga na mimi nikaona nichangie kitu kidogo, kana inaruhusiwa naomba Mufti uje nikukabidhi,” alisema Magufuli alipokuwa akizungumza katika Baraza la Eid el Fitri jijini Dar es Salaam jana. 
Baada ya kutamka maneno hayo, alishika begi dogo kama briefcase akampa msaidizi wake ambaye alilifungua na kuchomoa burunguti la noti na kumkabidhi Mufti, Sheikh Mkuu Zubeiry Ally. 
Hata hivyo haikufahamika kiasi cha fedha hizo. Kabla ya kutoa fedha hizo, awali akimkaribisha Rais Magufuli kuhutubia, Mufti Zubeiry aliwataka Waislamu kutumia Bakwata katika safari za hija zitakazogharimu Dola 3,800 kwa mtu mmoja. 
Awali Magufuli alikuwa ameahidi kitita cha Sh2 milioni kwa kijana aliyesoma dua katika sherehe hizo pamoja na kiasi kingine kama hicho kwa kundi la Kaswida lililotumbuiza. 
Katika hotuba yake, Dk Magufuli alisema Serikali yake ipo katika mchakato wa kurejesha heshima yake ingawa kuna watu wachache watakaoguswa kwa kuisababishia hasara Serikali. 
Rais Magufuli aliyekuwa mgeni rasmi katika baraza hilo la Eid el Firti alisema Tanzania ni nchi tajiri lakini baadhi ya watu wamesababisha watu waendelee kuwa masikini. 
“Tanzania hii ni tajiri sana, kila kitu kipo. Juzi mpaka wamegundua Helium tani za kutosha. Kila madini yapo hapa. Lakini kwa nini tuko masikini? Kwa nini watu wana shida? Ndiyo maana tumeamua kwa niaba yenu turudishe heshima yetu. tulete mabadiliko ya kweli na katika kufanya hayo wapo watu watakaoguswa, lakini ni wachache sana kuliko wale waliokuwa wanaguswa kwa kuibiwa, ni wachache waliokuwa wanadhulumiwa,” alisema Rais Magufuli. 
Alisema kwa miezi saba tangu alipochaguliwa kuingia madarakani Serikali yake imetekeleza mambo kadhaa ikiwa pamoja na kutoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari, kurudisha nidhamu ya watumishi wa umma, kudhibiti matumizi mabaya ndani ya Serikali, kuongeza mapato na mengineyo. 
“Pamoja na hatua hizo ni dhahiri kuwa bado tuna safari ndefu katika kutimiza yale tuliyokusudia na tuliyowaahidi Watanzania.  Naomba niwahakikishie kwamba dhamira ya kuwahudumia kwa nguvu zetu zote pamoja na vipaji vyote bado tunayo. Tuna sababu ya msingi na tuna imani kuwa Mungu yupo kuhakikisha kuwa tunaipeleka nchi yeti mbele...” alisema Rais Magufuli huku akiwataka waumini hao kuiombea Serikali. 
Aliwataka viongozi wa dini ya Kiislamu kuwahimiza waumini wao kushiriki katika shughuli za maendeleo hususani katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao utekelezaji wake umeanza mwezi huu.
“Tusipofanya kazi hatutapata pesa. Ndiyo maana wale waliozoea kupata fedha za bure wameanza kusema fedha zimeisha mifukoni. Hela haiji bila kufanya kazi,” alisema.
 Kuhusu mali za Waislamu zilizodhulumiwa, Rais Magufuli alisema atawasaidia kuzirejesha.
Alimpongeza Mufti wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Zubeiry akisema alikuwa mstari wa mbele katika kurejesha mali hizo kabla hata hajapewa cheo hicho. 
“Nakumbuka wakati nikiwa Waziri wa Ardhi, kabla hujawa Mufti, pamoja na viongozi wa Bakwata na wengine, ulifika ofisini kwangu ukieleza jinsi mali za Waislamu zilivyokuwa zinadhulumiwa. 

"Ninafamu pamekuwa na hiyo tabia ya baadhi ya viongozi wenye mali kuwatumia viongozi wa Bakwata na dini nyingine katika kuwarubuni na kuingia ubia, mali hizo baadaye huwa zinapotea kabisa,” alisema na kuongeza: 
“Tujitahidi kwa nguvu zote kusimamia mali hizi, zisije kuwa chanzo cha kuvunjika kwa amani. Tunapenda wawekezaji lakini wanachokiahidi hawatekelezi, haiwezekani. 
"Haiwezekani na wala haikubaliki kwa watu kwa ujanja wao na wakati mwingine kwa kutumia wanasheria wao kukalia mali za Waislamu. Mali za Waislamu lazima zirudi na za Wakristo zirudi ili amani iwepo.”
Baraza hilo lilihudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Katibu wa Bakwata Sheikh Suleiman Lolila na mabalozi wa nchi mbalimbali na waumini wa dini hiyo.

CHADEMA Yaandaa Vijana 4,000 wa Kuzuia mkutano wa CCM......Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA Ahojiwa na Jeshi la Polisi



BARAZA la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) limeendeleza msimamo wake wa kuzuia Mkutano Mkuu Maalum wa CCM, uliopangwa kufanyika Julai 23, mwaka huu mjini Dodoma.

Katika kuhakikisha linatimiza azma yake hiyo, baraza hilo limesema wanachama wake wapatao 4,000 wamejiandaa kushiriki kwenye shughuli hiyo.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, baada ya kuhojiwa kwenye Kituo Kikuu cha Polisi, Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Patrick ole Sosopi, alisema kuna vijana watakaotoka sehemu mbalimbali ili kuzuia mkutano wa CCM.
 
Sosopi alisema Bavicha watakwenda Dodoma kuzuia Mkutano Mkuu Maalum wa CCM kwa kile walichodai kusaidia Jeshi la Polisi kutekeleza amri yake ya kuzuia mikutano ya kisiasa hadi 2020.
 
Alisema pia kuna watu wamejitolea kutoa magari kwa ajili ya kuwabeba vijana hao ili kuwafikisha Dodoma kuunga mkono agizo la polisi.
 
Sosopi pia aliomba Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kutokana na kauli zao za vitisho walizozitoa dhidi ya Bavicha hivi karibuni.
 
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 4, mwaka huu, Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamad Shaka, aliionya Bavicha wasiende Dodoma kuzuia Mkutano Mkuu Maalum wa CCM kwa kuwa watatumia kila mbinu kuwazuia ili kulinda heshima ya chama chao.
 
Sosopi alisema wao hawataki matatizo wala vurugu bali wanachofanya ni kutii agizo la polisi kwa unyenyekevu.
 
"Mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu kwani Rais alipopiga marufuku mikutano ya kisiasa hadi 2020, CCM walichekelea wakiamini kuwa Chadema tumekomolewa lakini iweje sasa Jeshi la Polisi likubali kuruhusu mkutano wao wakati Chadema hata mikutano ya ndani tunazuiliwa?
 
"Hatutanii hata kidogo na wala CCM wasidhani kuwa hatutakwenda Dodoma lakini tunaliomba Jeshi la Polisi litende haki juu ya kauli za uchochezi kwani nilitegemea viongozi wa UVCCM wangekamatwa na jeshi hilo lakini tunaokamatwa ni sisi tu," alisema Ole Sosopi.
 
Akizungumzia suala la kuhojiwa na polisi jana, Ole Sosopi alisema alikuwa kituoni hapo kuhojiwa kwa kosa analodaiwa kufanya Juni 18, mwaka huu la kutoa kauli za uchochezi.
 
Sosopi alikamatwa mara ya kwanza Juni 26, mwaka huu mkoani Iringa na kusafirishwa hadi jijini Dar es Salaam na
kuhojiwa kwa kosa hilo katika shughuli ya mahafali ya wanachama wa Chadema waliomaliza vyuo vikuu.
 
Sosopi alisema baada ya kuhojiwa jana na polisi, anatakiwa kuripoti tena kituoni hapo Julai 18, mwaka huu.
 
Akizungumzia suala la Sosopi, mwanasheria wake, Frederick Kihwelo alisema Sosopi aliripoti kituoni hapo kwani anakabiliwa na tuhuma ya kutoa lugha ya uchochezi.
 
Alidai lengo la mteja wake ni kuhakikisha polisi wanatenda haki bila upendeleo kwani kazi yao kubwa ni kulinda usalama wa raia na mali zao
 
Alisema baada ya kuhojiwa na polisi jana, atatakiwa kufika tena kituoni hapo Julai 18, mwaka huu wakati huu upelelezi unafanyika na ushahidi kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaki ya Jinai (DPP) ili aamue kama kuna kesi ya kujibu au la.

Monday, May 30, 2016

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumanne ya May 31 .

Mke wa Trafiki Kinyogori Adaiwa Kukiri Kumuua Mumewe .


MKE wa askari polisi wa kikosi cha usalama barabarani (trafiki), Sajenti Ally Salum (Kinyogori) aliyeuawa hivi karibuni, inadaiwa amekiri kuhusika kwenye mauaji hayo, akidai ilitokana na mumewe kumuacha na kuoa mke mwingine.

Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa mwanamke huyo anashikiliwa na polisi kwa mauaji hayo yaliyofanyika nyumbani kwa Kinyogori, Mkuranga mkoani Pwani.

Wakati huo huo, Kamanda Sirro amezungumzia pia mauaji ya Anathe Msuya yaliyofanyika hivi karibuni Kigamboni na kusema polisi inaendelea kumtafuta msichana wa kazi za nyumbani aliyetoroka siku moja kabla ya kifo cha mwanamke huyo.

Anayetuhumiwa kuua mumewe 
Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu matukio mbalimbali ya uhalifu yaliyojitokeza jijini Dar es Salaam, Sirro alisema katika mahojiano ya awali mke wa Kinyogori amekiri kuhusika.

Kwa mujibu wa kamanda, mwanamke huyo ambaye hata hivyo hakutaja jina lake kwa sababu za kipelelezi, aliamua kumtuma mtu kutekeleza mauaji hayo baada ya mumewe kumwacha na kuoa mke mwingine.

“Ni jambo la kusikitisha kuona mtu anatoa uhai wa mtu sababu ya kuachwa. Tunawasihi wananchi kuepuka kujihusisha na matukio kama haya, eti sababu tu ya kuachwa wanawake wapo wengi na wanaume wapo wengi unaweza kuachwa na ukaolewa na ukaoa kuliko kuondoa uhai wa mtu,” alisisitiza Sirro.

Hata hivyo, Sirro alisema wanaendelea kuwahoji watuhumiwa hao ili waweze kuwataja watu wengine walioshirikiana nao kutekeleza tukio hilo baada ya kuonekana kuwepo kwa wahusika wengine.

‘Hausigeli’ asakwa 
Kuhusu mauaji ya Anathe aliyechinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, Kamanda Sirro alisema wanaendelea na jitihada za kumtafuta msichana huyo ahojiwe kuhusu tukio hilo.

Aidha alisema mtu mmoja anashikiliwa akituhumiwa kuhusika na tukio hilo huku polisi ikiwa imeandaa timu ya upelelezi itakayoshughulikia tukio hilo kufanikisha kuwakamata wote waliohusika na tukio hilo.

Sirro alisema msichana huyo aliondoka siku moja kabla ya tukio hilo la mauaji hivyo kupatikana kwake, kunaweza kusaidia polisi kujua kama kuondoka kwake kulikuwa salama au kuna kitu kimejificha.

“Msichana huyu tunaendelea kumsaka tujue kama aliondoka salama na kumhoji zaidi juu ya kuondoka kwake siku moja tu, tukio linatokea nina imani tutafanikiwa kumpata na wote waliohusika na kukomesha matukio haya,” alisema Sirro.

Mamia wajitokeza msibani 
Vilio na simanzi jana vilitawala wakati mamia ya wakazi wa Kibada Kigamboni na Salasala walipokuwa wakiuaga mwili wa marehemu Anathe Msuya (30), aliyeuawa Mei 25 nyumbani kwake kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana.

Mwili ulichukuliwa jana asubuhi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili na kupelekwa nyumbani kwake Kibada, kwa ajili ya kuagwa na majirani zake kabla ya kusafirishwa kwenda kuzikwa mkoani Arusha leo.

Akizungumza baada ya mamia kumuaga nyumbani kwa marehemu, mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Nyakwale Kibada, Said Pazi alisema kuwa wao kama majirani waliomba familia wapate fursa ya kumuaga jirani yao ambaye tangu ahamie ana muda wa miezi sita.

“Baada ya kuambiwa msiba upo Salasala tuliomba kama majirani na sisi tupatiwe fursa ya kuuaga mwili wa ndugu yetu ambaye alihamia mwaka jana… kwa kweli msiba wake umetusikitisha sana” alisema.

Akizungumzia tukio hilo alisema kuwa mtoto wa marehemu huyo, Allan Kimario (4) aliwataarifu majirani kuwa mama yake haamki na ndipo walipofika wakakuta ameuawa.

Mwenyekiti huyo alitoa pole na kusema atahakikisha wanaimarisha ulinzi na kuhimiza wenye viwanja ambavyo havijajengwa, wavifanyie usafi ili kuondoa vichaka ambavyo ni hatari kwa usalama.